Yanga SC yatamba wapo tayari kuivaa CR Belouizdad

KLABU BINGWA AFRIKA Yanga SC yatamba wapo tayari kuivaa CR Belouizdad

Zahoro Mlanzi • 22:00 - 14.11.2023

Timu hiyo inatarajia kuanzia kampeni yao hatua ya makundi ugenini katika mechi iliyopangwa kuchezwa kati ya Novemba 24 au 25

Makamu wa Rais wa Klabu ya Yanga, Arafat Hajji, amesema mipango yote kuhusu mechi ya CR Belouizdad imekamilika na kwamba wanachofanya ni kwenda na ratiba tu waliyoandaa.

Mbali na hilo, Arafat amesema hadi sasa Yanga wanajua watafikia wapi na wataondoka siku gani lakini kwasasa kazi bado ipo kwa benchi la ufundi kuendelea kuandaa kikosi wakiwa hapa Tanzania kwa siku kadhaa.

Yanga wanatarajia kuanza kampeni yao katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika hatua ya makundi ugenini dhidi ya CR Belouizdad mechi ambayo imepangwa kuchezwa kati ya Novemba 24 au 25.

Akizungumza na Pulsesports jijini Dar es Salaam, Arafat amesema wao kama uongozi huwa wanafanya mambo yao mapema na hususani kwa nchi kama Algeria tayari wana uzoefu napo.

"Sisi tupo tayari katika upande wa maandalizi na mipangilio yote ipo tayari, tunakwenda kwa mujibu wa ratiba na kila kitu kitafanyika kwa wakati wake kama tulivyopanga," amesema.

Amesema msimu huu wamejipanga kufanya vizuri na kufika mbali kwenye michuano ya hiyo kama walivyofanya msimu uliopita katika mashindano ya Kombe la Shirikisho.

Aidha Arafat hakusita kulia na ratiba ya timu ya taifa ambapo amesema kuna changamoto katika maandalizi ya kikosi hasa kwenye upande wa ratiba hiyo.

Amesema mechi za timu za taifa nyingine zitamalizika Novemba 21 na wapo baadhi ya wachezaji wao watakuwa na mechi hadi kufikia Novemba 22 hivyo itakuwa ni changamoto kwa upande wa kocha kuwa na kikosi chote kamili.

"Unajua hii mechi ya Uarabuni tunacheza kati ya Novomba 24 hadi 25 lakini kuna baadhi ya wachezaji walioko kwenye timu za taifa hatutawapata hadi Novemba 22," amesema.

Katika michuano hiyo, Yanga imepangwa kuanza ugenini dhidi ya CR Belouizdad na kisha watarejea nyumbani Desemba 2 kumenyana na Al Ahly ya Misri.

Mechi hizo zitafuatiwa na mechi dhidi ya Medeama FC nyumabani Desemba 9.