Yanga SC yasaini mkataba mil. 900/- na NIC

© Kwa Hisani

KANDANDA Yanga SC yasaini mkataba mil. 900/- na NIC

Zahoro Mlanzi • 21:00 - 09.10.2023

Hayo ni makubaliano ya muda wa miaka mitatu ambapo ni sh. milioni 900 zitapatikana kwa muda wa miaka mitatu.

Klabu ya Yanga, imeingia makubaliano na Kampuni ya Bima ya NIC kwa ajili ya kudhamini tuzo za mchezaji bora wa mwezi.

Hayo ni makubaliano ya muda wa miaka mitatu ambapo ni sh. milioni 900 zitapatikana kwa muda wa miaka mitatu.

Akizungumza kuhusu hilo, Rais wa Klabu ya Yanga, Injinia Hersi Said, amesema hiyo ni fursa kwao itakayotumiwa vyema na wachezaji kuendelea kutimiza majukumu yao uwanjani huku wakiendeleza mahusiano mazuri ya kibiashara na NIC.

“Makubaliano haya ya kibiashara kimsingi yanakwenda kunufaisha pande zote. Yanga inakwenda kupata kiasi cha shilingi milioni 900 kwa kipindi cha miaka mitatu. NIC nao wanapata fursa ya biashara yao kutangazwa kwa ukubwa.

“Tunaelewa kwanini wamechagua kufanya kazi na sisi. Tuna wachezaji bora zaidi ambao huwezi kuwapata kwenye klabu nyingine. Wachezaji hawa wana ushawishi mkubwa nje na ndani ya uwanja. Ushawishi wao ni chachu ya kutangaza biashara,” amesema Hersi.

Kwa upande wa Mtendaji Mkuu wa NIC, Elihuruma Doriye, amesema: “Historia imeandikwa baada ya taasisi mbili zenye chapa ya kihistoria kwa Tanzania kuingia makubaliano ya kibiashara kwa miaka mitatu.

“Huwezi kuzungumzia bima bila kuitaja NIC, na katika soka Yanga ni nembo ya soka kwa Tanzania akiwa bingwa wa kihistoria. Tunayo furaha kubwa kupata fursa ya kufanya biashara na taasisi kubwa kama hii. Kwa upande wetu NIC imepewa hadhi ya kuaminika.”