Yanga SC kuwania Tuzo ya Klabu Bora Afrika

Tuzo za CAF Yanga SC kuwania Tuzo ya Klabu Bora Afrika

Mark Kinyanjui • Zahoro Mlanzi • 18:40 - 01.11.2023

Yanga wanawania tuzo hiyo pamoja na miamba ya Afrika, Al Ahly ya Misri, USM Alger ya Algeria na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Klabu ya soka ya Yanga ya Tanzania, imeingia kwenye kinyang'anyiro cha kuwania tuzo ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ya kipengele cha Klabu Bora Afrika.

Yanga wanawania tuzo hiyo mbele ya miamba ya Afrika, Al Ahly ya Misri ambao ni mabingwa wa Klabu Bingwa Afrika na USM Alger ya Algeria ambao ni mabingwa wa Kombe la Shirikisho.

Wengine ni Mamelodi Sundowns, Marumo Gallant zote (Afrika Kusini) Wydad Casablanca na Raja Casablanca zote (Mororcco), Esperance de Tunis (Tunisia), Asec Mimosas (Ivory Coast) na CR Beluizdad ya Algeria.

Yanga wamewekwa katika kipengele hicho mara baada ya kushinda mataji yote ya ndani yakiwemo Ligi Kuu na Kombe la FA huku pia wakitinga fainali ya michuano ya Shirikisho Afrika ambapo walipoteza taji mbele ya USM Alger.

Katika upande mwingine, Kipa namba moja wa timu hiyo, Djigui Diarra raia wa Mali, ameteuliwa kuwania tuzo ya Kipa Bora Afrika akichuana na Andre Onana wa Manchester United na Edward Mendy kipa wa zamani wa Chelsea.

Diarra anawania tuzo hiyo baada ya kuonesha kiwango bora msimu uliopita ambapo aliisaidia timu yake kupata mafanikio makubwa ya michuano ya ndani lakini pia kuipeleka timu yake kwenye hatua ya fainali ya Shirikisho Afrika.

Lakini pia ametajwa katika kipengele cha kuwania Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka kwa wachezaji wanaocheza Ligi ya Ndani.

Ikumbukwe Diarra alikuwa ndio nyota wa mchezo wa fainali mkondo wa pili uliochezwa Algeria ambapo Yanga walishinda 1-0.

Mbali na Onana na Mendy, makipa wengine wanaowania tuzo hiyo ni Mohamed El Shenawy wa Al Ahly, Ronwel Williams wa Mamelod Sundowns, Yasin Bounou, Landing Badji, Pape Mamadou SY, Oussama Benbot na Youssef El Motie.

Katika vipengele vingine, timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', imeingia katika kichang'anyiro cha kuwania tuzo ya Timu Bora ya Taifa ya mwaka.

Stars itashindana na mabingwa wa Afrika, Senegal, Namibia, Msumbiji, Morocco, Mauritania, Guinea ya Ikweta, Guinea Bissau ya Gambia na Cape Verde.

Pia mshambuliaji wa zamani wa Yanga ambaye kwasasa anakipiga na Pyramid ya Misri, Fiston Mayeke, ameteuliwa kuingia katika vipengele viwili ambavyo ni Mchezaji Bora wa mwaka lakini pia ameingia kwenye tuzo ya kuwania Mchezaji Bora wa mwaka kwa wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani.

Tuzo hizo zinatarajiwa kutolewa Desemba 11 nchini Mororcco ambapo washindi watajulikana na kukabidhiwa tuzo zao.

Tags: