Uwanja wa Mkapa upo tayari kwa African Super League

© Kwa Hisani

KANDANDA Uwanja wa Mkapa upo tayari kwa African Super League

Zahoro Mlanzi • 22:00 - 09.10.2023

Kampuni ya Formula 360, itafunga mfumo wa matangazo ya kidijitali ambao utaanza kufanya kazi rasmi Oktoba 20

Ukarabati wa awamu ya kwanza unaoendelea katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, umefikia asilimia 95 na asilimia tano zilizobaki zinatarajiwa kukamilika ndani ya siku tano zijazo.

Akikagua ukarabati huo leo, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro, amesema tayari vyumba vinne vya wachezaji, sehemu ya kuchezea, vyumba vya waamuzi, afya na eneo la video za marejeo (VAR) umekamilika.

"Tayari taa za kisasa 320 za mfumo wa LED zimefungwa na kuna huduma ya mtandao wa bure kabisa kwa ajili ya watazamaji wa mechi ambao tutauzindua kati ya tarehe 17 hadi 19 mwezi huu kabla ya mchezo wa ufunguzi wa African Football League kati ya Simba na Al Alhy ya nchini Misri Oktoba 20," amesema Ndumbaro.

Ameongeza katika eneo la watu mashuhuri na sehemu ya Waandishi wa Habari kazi iliyobakia ni ndogo ambayo itamalizika ndani ya siku hizo tano akiongeza kuwa mfumo wa sauti uwanjani tayari umerekebishwa.

Dkt. Ndumbaro amesema Kampuni ya Formula 360, itafunga mfumo wa matangazo ya kidijitali ambao utaanza kufanya kazi rasmi Oktoba 20 huku akisistiza kuwa baada ya mchezo huo, ukarabati mkubwa wa awamu ya pili utaendelea.

Tags: