Simba SC yapigwa 1-0 ugenini na Wydad Casablanca

KANDANDA Simba SC yapigwa 1-0 ugenini na Wydad Casablanca

Na Zahoro Mlanzi • 08:00 - 10.12.2023

Matokeo hayo yameifanya Simba kushika mkia kutoka Kundi B ikiwa na alama 2 baada ya kucheza mechi tatu

Timu ya Simba SC, imekubali kichapo cha bao 1-0 ugenini kutoka kwa Wydad Casablanca ya Morocco katika mfululizo wa mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi.

Bao la ushindi la Wydad, limefungwa dakika ya mwisho ya muda wa nyongeza na mshambuliaji, Zakaria Draoui baada kupokea mpira ulioanguka ndani ya eneo la hatari na kushindwa kuokolewa na wachezaji wa Simba.

Katika mchezo huo ambao ulikuwa ni wa tatu kwa kila timu, nafasi zilitengeneza kwa kila upande lakini milango ilikuwa ni migumu kiasi kwamba wawili hao walikuwa wanakaribia kugawana alama moja.

Kipa wa Simba, Ayoub Lakred, angeweza kuibuka shujaa kama matokeo yangebaki suluhu baada ya kuokoa penalti ya Yahya Jebrane kwenye kipindi cha kwanza.

Huu unakuwa ni ushindi wa kwanza kwa Wydad na Kocha wao, Adel Ramzi ambaye alikuwa katika msukumo mkubwa wa kupingwa na mashabiki wa timu yake baada ya mfululizo wa matokeo mabovu.

Kwa upande wa Simba, kipigo hiki ni cha kwanza kwenye michuano ya kimataifa msimu huu lakini pia ni mechi ya kwanza kwa Kocha, Abdelhak Benchikha kufungwa akiwa kocha wa timu hiyo tangu alipotangazwa wiki iliyopita.

Msimamo wa kundi hilo la B, kwasasa unaonesha, Asec Mimosa wakiwa vinara baada ya kukusanya alama 7, hii ni baada ya kuwafunga Jwaneng Galaxy kwa mabao 2-0 kwenye mchezo uliotangulia mapema.

Jwaneng wao wanasalia nafasi ya pili wakiwa na alama 4 na Wydad sasa wanapanda hadi nafasi ya tatu wakiwa na alama 3.

Klabu ya Simba wao wanaburuza mkia wakiwa na alama zao 2 baada ya kushuka dimbani mara tatu.

Mchezo unaofuata kwa Simba utakuwa ni wa nyumbani dhidi ya Wydad ambao utapigwa Desemba 19.

Tags: