Simba SC yakiri Yanga wagumu kufungika

Ligi Kuu Simba SC yakiri Yanga wagumu kufungika

Zahoro Mlanzi • 21:45 - 03.11.2023

Yanga wana wachezaji wengi wazuri lakini wao hawahofii mchezaji mmoja mmoja bali timu nzima.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Soka ya Simba, Ahmed Ally, amekubali 'mziki' wa Yanga kwa kusema ni wagumu kufungika kwasababu wanacheza kitimu.

Hayo ameyasema jijini Dar es Salaam wakati akiwa kwenye shughuli za hamasa kuelekea mechi ya Kariakoo Derby itakayopigwa Jumapili, Uwanja wa Mkapa.

Ally amesema Yanga wana wachezaji wengi wazuri lakini wao hawahofii mchezaji mmoja mmoja bali timu nzima.

Amesema kama watafanikiwa kushinda mechi ya Jumapili basi njia itakuwa nyeupe kwao kulitwaa taji msimu huu na kuwapokonya Yanga ambao wamelishikilia kwa misimu miwili mfululizo.

"Yanga ni wapinzani wagumu kweli kweli, hii itakwenda kuwa mechi ngumu na kubwa yenye ushindani. 

Kama tutafanikiwa kupata alama tatu kwenye mechi hii basi ni rasmi mbio za ubingwa zitakuwa upande wetu," amesema Ally.

Ally ametaja baadhi ya vitu ambavyo anaona kuwa ni bora kwa Yanga kuwa ni kujituma pindi timu inapokuwa haina mpira na jinsi wanavyotengeneza nafasi za kufunga.

Hata hivyo Ally almesema wao wanajiandaa vizuri na watashinda kama walivyofanya mara ya mwisho walipokutana kwenye ligi.

Simba wanatarajiwa kuwa wenyeji kuwakaribisha Yanga kwenye muendelezo wa Ligi Kuu Bara mzunguko wa nane na mechi hiyo itapigwa saa 11 jioni.

Wakati huo huo, Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Karim Boimanda, amesema kuwa mageti yatakuwa wazi kuanzia saa nne asubuhi ili kuepusha msongamano.

Tags: