Simba SC yaichimba mkwara Al Ahly

FOOTBALL Simba SC yaichimba mkwara Al Ahly

Zahoro Mlanzi • 22:00 - 13.10.2023

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Oktoba 20, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar, kisha marudiano Oktoba 24 nchini Misri.

Ikiwa imebaki wiki moja kabla ya Simba SC haijashuka uwanjani kuumana na Al Ahly katika mchezo wa ufunguzi wa michuano ya African Football League (AFL), uongozi wa timu hiyo, umesema watawaonesha wapinzani wao kwamba wao ni timu ya aina gani.

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Oktoba 20, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar, kisha marudiano Oktoba 24 nchini Misri.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mashindano ya AFL Simba Beach Bonanza Buguruni, Dar es Salaam,Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmedy Ally, amesema wana malengo ya kuhakikisha wanakwenda kushindana na sio kushindwa, hivyo wana kila sababu ya kupata matokeo mazuri katika mchezo huo ambao ni muhimu kwao kushinda.

“Tuna malengo makubwa ya kuhakikisha tunafanya vizuri katika mashindano haya mapya, hatuna malengo ya kwenda kushindwa wala kwenda kushiriki tu, bali kwenda kushindana haswa.

“Tunakwenda kushindana, tunataka kwenda kulionesha Bara la Afrika kuwa sisi ni timu kubwa ambayo ina malengo makubwa ya kutaka kufanya makubwa zaidi,” amesema kiongozi huyo.

Akizungumzia kuhusu AFL Simba Beach Bonanza, amesema itahusisha timu zao za matawi mbalimbali ikiwa ni katika kuhamasisha wanachama na mashabiki wao kuelekea mchezo huo.

"Simba inashirikisha michezo mbalimbali kama ilivyo sports club (timu ya michezo) ndio maana mnaona tunafanya bonanza kama la ufukweni.

Lakini pia huu ni mwanzo wa mashindano ya matawi kuelekea Simba Day ya mwakani," ametoa zaidi ufafanuzi Mkurugenzi wa Wanachama na Mashabiki wa timu hiyo, Hamisi Kissiwa.

"Bingwa wa AFL Simba Beach Bonanza atapata kombe." amesema.

Tags: