Robertinho amtaja Kibu kufungwa na Yanga

KANDANDA Robertinho amtaja Kibu kufungwa na Yanga

Na Zahoro Mlanzi • 20:22 - 06.11.2023

Wapinzani wetu walikuwa bora hasa kipindi cha pili, hata hivyo timu yangu ilianguka zaidi baada ya kuondokewa na mchezaji wetu muhimu

Baada ya kupokea kipigo cha mabao 5-1 kutoka kwa watani zao wa jadi, Yanga, Kocha wa timu ya Simba SC, Roberto Oliviera 'Robertinho', amesema kuumia kwa mshambuliaji wake, Kibu Denis kuliathiri mchezo kwa upande wao.

Mchezo huo uliohudhuriwa na maelfu ya mashabiki, ulipigwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Akizungumza na Pulsesports baada ya mchezo huo, Robertinho, amesema wapinzani wao walitumia nafasi zao vizuri na kufunga mabao hayo matano lakini wao kuna muda waliushika vizuri mchezo hasa Kibu alipokuwa uwanjani.

Kwenye mchezo huo, Kibu alifanyiwa mabadiliko dakika ya 56 kutokana na jeraha la mguu alilopata baada ya kugongana na mlinda lango wa Yanga, Djigui Diarra na wakati huo matokeo yakiwa 1-1.

Nafasi ya Kibu ilichukuliwa na Luis Miquissone ambaye mchango wake haukuonekana uwanjani na alishindwa kuinusuru klabu yake na kipigo hicho.

"Wapinzani wetu walikuwa bora hasa kipindi cha pili, hata hivyo timu yangu ilianguka zaidi baada ya kuondokewa na mchezaji wetu muhimu," amesema.

Katika hatua nyingine, kocha huyo, ametetea uamuzi wake wa kumuanzisha golini kipa wao namba moja, Aishi Manula ambaye hakucheza kwa kipindi kirefu kutokana na majeraha.

Mara ya mwisho Manula kucheza mechi ya ushindani ilikuwa ni Aprili ambapo alikuwa akisumbuliwa na majeraha ya nyama za paja.

Baada ya kukaa nje kwa zaidi ya miezi sita, jambo la kushangaza kwa watu wengi ilikuwa ni kuona kipa huyo akianza mbele ya Ally Salim ambaye alikuwa langoni katika mechi mbili zilizopita dhidi ya Yanga na Simba walifpata ushindi.

Hata hivyo wazo la kumuanzisha Manula katika mchezo huo, limeonekana kupingwa na wadau mbalimbali wa soka na ndipo Robertinho alipoamua kulitolea maelezo.

"Ni kweli Manula alikuwa nje kwa muda mrefu lakini tulishauriana na viongozi wenzangu wa benchi la ufundi baada ya kuridhishwa na maendeleo yake," amesema.

Ushindi huo umeiweka Yanga kileleni wakiwa na alama 21 huku Simba wakibaki kwenye nafasi ya 3 na alama zao 18 na mchezo mmoja mkononi, Azam ikishika nafasi ya pili kwa alama 19.

Tags: