Rais wa Yanga 'amfuata' Chivaviro Afrika Kusini

LIGI KUU Rais wa Yanga 'amfuata' Chivaviro Afrika Kusini

Na Zahoro Mlanzi • 17:21 - 12.11.2023

Yupo nchini humo kwa takribani siku tatu na alikwepo uwanjani kushuhudia 'Soweto Derby' mechi kati ya Kaizer Chiefs walioshinda bao 1-0 dhidi ya Orlando Pirates Jumamosi.

Katika kipindi hiki cha mapumziko ya kupisha timu za taifa, Injinia Said Hersi yeye hakupumzika badala yake yupo nchini Afrika Kusini akikamilisha jambo.

Hersi yupo nchini humo kwa takribani siku tatu na alikwepo uwanjani kushuhudia 'Soweto Derby' mechi kati ya Kaizer Chiefs walioshinda bao 1-0 dhidi ya Orlando Pirates Jumamosi.

Lakini kabla hata ya mchezo huo, Ijumaa, Hersi alikutana na uongozi wa juu kabisa wa Kaizer Chief ukiongozwa na mmiliki, Kaizer Motaung.

Licha ya kuwa mambo mengine waliyozungumza yanabaki kuwa siri lakini moja kati ya agenda ya kikao chao ilikuwa ni kulizungumzia jina la mshambuliaji, Ranga Chivaviro anayekipiga na timu hiyo 'Amakhosi' kwa sasa.

Mshambuliaji huyo alikuwa Marumo Gallants msimu uliopita na alikuwa ni moja kati ya wachezaji muhimu walioisadia klabu yake kufika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika licha ya kuwa walishuka daraja.

Chivaviro alifunga mabao matano kwenye msimu wa michuano hiyo nyuma ya Fiston Mayele aliyekuwa Yanga ambaye sasa yupo Pyramid ya Misri.

Yanga watafungua pazia mechi za kimataifa ugenini Novemba 25 dhidi ya CR Beluizdad ya Algeria kisha watawakaribisha Al Ahly, Desemba 2 kabla ya kucheza na Medeama ya Ghana.

Katika mchezo wa Soweto Dery, Hersi alikuwa jukwaani sambamba na Rais wa CAF, Patrice Motsepe na Rais wa FIFA, Gianni Infantino, huku Chivaviro akianza na kudumu uwanjani kwa dakika 61 kabla ya kufanyiwa mabadiliko wakati timu yake ikiwa nyuma kwa bao 1-0.