Rais huyo aliahidi kwenye safari ya Taifa Stars kila goli atakuwa anatoa sh. milioni 10
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametimiza ahadi ya kuipatia timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ sh. milioni 10 kutokana na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Niger.
Timu hiyo jana imeibuka na ushindi huo katika mchezo uliopigwa nchini Morocco kutokana na Niger nchini kwao kuwa na machafuko ya kisiasa.
Fedha hizo zimewasilishwa na Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa wakati wa kuipokea timu hiyo baada ya kuwasili leo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam.
“Kama mnavyojua Mheshimiwa Rais aliahidi kwamba kwenye safari ya Taifa Stars kila goli atakuwa anatoa sh. milioni 10” amesema Msigwa.
Pamoja na hilo Rais Samia amelipia eneo la mzunguko lenye takribani viti 30,000 kwajili ya Watanzania watakaofika kuishangilia timu hiyo Jumanne kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa.
Msigwa amesema hiyo ni sehemu ya kampeni maalum iitwayo “oparesheni Samia Kombe la Dunia” kwajili ya kuhamasisha timu kufuzu Kombe la Dunia.
Mchezo huo ni wa kwanza kwa Stars kutoka Kundi E ambapo sasa Ina kibarua kigumu cha kuumana na Morocco.
Bao la ushindi katika mchezo huo lilifungwa kipindi cha pili dakika ya 56 na Charles M'mbobwa ambaye anacheza soka la kulipwa katika Klabu ya Macarthur ya nchini Australia na alikuwa akicheza mechi yake ya kwanza akiwa na Stars.