Rais Samia achangia sh. milioni 500 harambee kusaidia timu za Taifa

Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Suluhu, akiwa katika majukumu yake michezoni

KANDANDA Rais Samia achangia sh. milioni 500 harambee kusaidia timu za Taifa

Na Zahoro Mlanzi • 20:00 - 11.01.2024

Fedha zitakazopatikana katika harambee hiyo ni kwa ajili ya maandalizi ya timu mbalimbali za Taifa zitakazoshiri mashindano ya kimataifa ya mwaka huu

Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amechangia sh. milioni 500 na kuwataka wadau wengine kuzisaidia timu za taifa za michezo mbalimbali zinazotarajia kushiriki michuano ya kimataifa mwaka huu.

Hayo yalisemwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati wa harambee maalumu iliyofanyika jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kukusanya fedha ambazo zitasaidia timu ambazo zinatarajia kuwakilisha nchi ikiwemo timu ya taifa Tanzania ya 'Taifa Stars' ambayo kwasasa ipo Ivory Coast ikishiriki michuano ya Afcon.

Hafla hiyo iliongozwa na Majaliwa, ambaye alimuwakilisha Rais Samia kama mgeni rasmi na zilipatikana jumla ya shilingi bilioni 3.7 kutoka kwa wadau mbalimbali huku lengo ikiwa ni kukusanya kiasi cha sh. bilioni 10 ndani ya miezi mitatu.

"Michezo ni jukumu letu, ni jukumu la Serikali na jukumu la Watanzania, michezo ni gharama, serikali imejitahidi kuhamasisha na timu zimetuitikia lakini tunafika mahala tunakwama kutokana na uchache wa bajeti, wito wangu na ombi langu kwenu tuchangie timu zetu ili ziende kuwakilisha jina la Tanzania," alisema Majaliwa kwa niaba ya Rais Samia.

Harambee hiyo iliandaliwa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo iliyo chini ya Waziri, Dkt. Damas Ndumbaro ambaye alitoa shukrani zake za dhati kwa wadau mbalimbali waliojitokeza na wanaoendelea kuchangia.

Dkt. Ndumbaro amesema Serikali imejikita katika sekta ya michezo na sanaa kwasababu zipo fursa nyingi za kibiashara na uchumi ambazo zinaweza kuwanufaisha watu binafsi na nchi kwa ujumla.

"Kwa sasa michezo na sanaa ni biashara na uchumi, hivyo tupo katika mchakato na tutawatajia Watanzania wajue kuhusu takwimu za uchumi katika sekta ya michezo," amesema.

Ndani ya mwaka 2024 ukiachana naTaifa Stars kushiriki Afcon nchini Ivory Coast, lakini pia timu ya Taifa ya Wanawake 'Twiga Stars' inatarajia kushiriki michuano ya WAFCON nchini Morocco mapema Juni.

Pia mwaka huu kutakuwa na mashindano ya Olimpiki ambayo yanatarajia kufanyika Paris, Ufaransa ambapo yanatarajiwa kuanza Julai na kumalizika Agosti ambapo wanamichezo mbalimbali wanatarajiwa kushiriki wakiwemo wale wa kutoka Tanzania.

Tags: