Rais Dkt. Samia kutoa mil. 10/- kila bao kwa Simba SC ikiifunga Al Ahly

© Kwa Hisani

KANDANDA Rais Dkt. Samia kutoa mil. 10/- kila bao kwa Simba SC ikiifunga Al Ahly

Zahoro Mlanzi • 22:00 - 18.10.2023

Mchezo huo utahudhuriwa na ugeni mzito wa viongozi wa soka kutoka kona mbalimbali duniani.

Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kutoa zawadi ya sh. milioni 10 kwa kila bao ambalo timu ya Simba SC itafunga na kushinda mechi kwenye michuano ya AFL ambapo Ijumaa itaumana na Al Ahly ya Misri.

Mchezo huo utahudhuriwa na ugeni mzito wa viongozi wa soka kutoka kona mbalimbali duniani utachezwa kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es salaam kuanzia saa 12 jioni.

Baadhi wageni ambao wanatarajiwa kuhudhuria ni pamoja na Kocha wa zamani wa Klabu ya Arsenal, Arsene Wenger ambaye ataambatana na Raisi wa FIFA, Gianni Infantino na Rais wa CAF, Patrice Motsepe.

Wengine ni pamoja na viongozi wengine waandamizi wa mashirikisho ya mpira Afrika ambao watalakiwa na viongozi wa ngazi za juu wa Serikali ya Tanzania.

"Wakati nakuja huku niliongea na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na akaniambia nenda kawahamasishe wana-Simba na watanzania kwa ujumla kuwa mechi hii ni ya Watanzania," amesema Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa wakati alipoungana na wanachama na mashabiki wa timu hiyo Mbagala kuendelea na hamasa.

Amesema ingawaje hakuwa amesema kabla ila Rais Samia ameahidi kutoa sh. milioni 10 kwa kila bao katika mechi ambayo Simba itashinda katika michuano ya AFL.

Amesema kutokana na ubora na ukubwa wa michuano hiyo ndio maana ameamua kuanzia na sh. milioni 10 na kwamba pia ataenda kuwatembelea wachezaji kambini kwao.

Ameongeza uwanja huo umeshakamilika kwa asilimia 100 na siku hiyo ya mchezo kuna vitu vitaonekana ambayo havijawahi kufanyika Tanzania.

Hii si mara ya kwanza kwa Dkt. Samia kuunga mkono juhudi za michezo nchini kwani msimu uliopita alizizawadia zaidi ya sh. milioni 100 timu za Simba na Yanga ambazo kwa pamoja zilikuwa zikiiwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa.

Mbali na klabu lakini pia zawadi hizo zilifika hadi kwenye timu za taifa ambazo zilikuwa zikishiriki michuano mbalimbali.

Tags: