Mudathir aweka rekodi ya kufunga bao la mapema

Kiungo wa Yanga, Mudathir Yahaya, akishangilia moja ya bao lake

LIGI KUU Mudathir aweka rekodi ya kufunga bao la mapema

Na Zahoro Juma • 20:13 - 20.02.2024

Ni lile alilofunga mwishoni mwa wiki sekunde ya 44 dhidi ya KMC.

Kiungo wa timu ya Yanga SC, Mudathir Yahya, ameshikilia rekodi ya kufunga bao la mapema zaidi hadi sasa msimu huu kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Bodi ya Ligi kuu Tanzania Bara.

Bao lililoweka rekodi la Mudathir ni lile alilofunga kwenye mchezo wa ligi dhidi ya KMC Jumamosi ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Mudathir ndiye alikuwa wa kwanza kufunga bao katika mchezo huo, akifunga sekunde ya 44 tu ya mchezo na bao hilo lilidumu hadi timu hizo zinakwenda kwenye vyumba vya mapumziko.

Bao ambalo awali lilikuwa linashikilia rekodi lilikuwa ni la kiungo wa Azam, Sospter Bajana ambaye alifunga kwenye sekunde ya 54 wakati timu yake inacheza na JKT Tanzania.

Katika mchezo huo, Mudathir alifunga bao lingine la katika kipindi cha pili na bao la tatu kwa Yanga lilifungwa na kiungo, Pacome Zouzoua.

Mudathir ambaye kashawawi kucheza Azam na Singida United, amekuwa katika kiwango kizuri kwenye mechi za hivi karibuni tangu kurejea kwa ligi akifunga mabao manne katika mechi sita zilizopita.

Hadi sasa kwenye ligi ana jumla ya mabao sita idadi ambayo hajawahi kufikisha kwa msimu mmoja tangu alipoanza maisha yake ya soka ndani ya Ligi Kuu Bara.

Tags: