Mexime apigia hesabu kumaliza ‘Top 4’

KANDANDA Mexime apigia hesabu kumaliza ‘Top 4’

Zahoro Juma • 21:26 - 05.02.2024

Katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Ihefu inashika nafasi ya tatu kutoka mkiani ikiwa na alama 13

Kocha Mkuu wa kikosi cha Ihefu FC, Mecky Mexime, amesema kwa jinsi anavyoiona timu yake anaamini msimu huu kuna uwezekano wakapata moja kati ya nafasi za kucheza michuano ya kimataifa msimu ujao.

Mexime ameyasema hayo akiwa na kikosi chake kilichoweka kambi yao ya maandalizi Arusha kuelekea mechi za Ligi Kuu ambapo Februari 12 itacheza na Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Manungu, Morogoro.

"Kwasasa kazi yangu kubwa ni kuunganisha hiki kikosi kiweze kucheza kwa pamoja na kwa uelewano mkubwa, kikosi kina wachezaji wengi wapya na wazuri na mimi pia ni kocha mpya hivyo nashukuru tumetumia muda wetu vizuri katika maandalizi," amesema.

Ameongeza kambi yao ya maandalizi tangu mkoani Mbeya na kisha Arusha imekuwa ni yenye tija kubwa na anaimani ya kufanya vizuri mara baada ya mechi za mashindano kurejea.

Mexime alijiunga na Ihefu mapema Desemba baada ya kufungashiwa virago vyake na timu ya Kagera Sugar kutokana na mfululizo wa matokeo mabovu.

Kocha huyo ambaye pia aliwahi kuifundisha Mtibwa Sugar, aliingia Ihefu kuziba nafasi iliyochwa wazi na Kocha, Moses Basena baada ya kutimuliwa kutokana na mwenendo wa kusuasua wa timu hiyo wakati ligi inaendelea.

Katika msimamo wa ligi hiyo, Ihefu inashika nafasi ya tatu kutoka mkiani ikiwa na alama 13.

Tags: