Matola aichimba  mkwara Singida FG

KANDANDA Matola aichimba mkwara Singida FG

Zahoro Mlanzi • 20:41 - 09.01.2024

Kocha huyo msaidizi wa Simba, anajivunia rekosi nzuri ya timu yake mbele ya timu hiyo

Kocha Msaidizi wa timu ya Simba, Seleman Matola, amesema watatumia wembe ule ule kuendelea kuwanyoa wapinzani wao katika michuano ya Mapinduzi Cup mwaka huu.

Hayo ameyasema kwenye mkutano na waandishi wa habari wakati timu yake ikijiandaa kukabiliana na Singida FG kwenye mchezo wa nusu fainali ambao unatarajia kuchezwa kesho Uwanja wa New Amani Complex kuanzia saa 2: 15 usiku.

Simba imefika katika hatua hiyo baada ya kuifunga Jamhuri bao 1-0 katika mchezo wa robo fainali huku Singida FG wakifanya kazi ya ziada kuifunga Azam kwa mabao 2-1.

Matola amesema malengo yao ni kufanya vizuri kwenye michezo yao yote katika michuano hiyo.

"Tuna malengo ya kuendelea kufanya vizuri katika michezo yetu yote kama tulivyofanya kwenye michezo iliyopita," amesema.

Katika mchezo huo, Simba itaingia ikiwa inajiamini kwa asilimia kubwa hasa baada ya kuwafunga Singida FG katika michezo mitatu ya mashindano tofauti waliyokutana msimu huu.

Singida FG wanajivunia rekodi yao ya kufanya vizuri tangu walipoanza kushiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza msimu uliopita ambapo walitinga fainali kabla ya kufungwa na Mlandege.

Hata msimu huu wamekuwa katika kiwango kizuri huku mshambuliaji wa raia wa Kenya, Elvis Rupia akiwa ni kinara wa mabao akifunga manne hadi sasa.

Macho na masikio ya mashabiki wengi yanatarajia kuelekezwa kwa kiungo mpya wa Simba raia wa Senegal, Babacar Sarr ambaye katika mchezo dhidi ya Jamhuri alicheza kwa dakika 20 tu.

Tags: