Makocha wa Taifa Stars, Morocco wachimbana mkwara

KANDANDA Makocha wa Taifa Stars, Morocco wachimbana mkwara

Zahoro Mlanzi • 08:30 - 21.11.2023

Mchezo huo unatarajiwa kuanza saa 4 usiku Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam

Makocha wa timu za Taifa za Tanzania 'Taifa Stars', Adel Amrouche na wa Morocco,Walid Regragui, kila mmoja ametamba ataibuka na ushindi watakapokutana katika mchezo wa kesho wa kufuzu Kombe la Dunia 2026.

Mchezo huo unatarajiwa kuanza saa 4 usiku Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam ambapo mashabiki watakaokaa viti vya mzunguko hawatalipa kiingilio kutokana na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kununua tiketi zote za eneo hilo.

Mchezo huo wa Kundi E ni wa pili kwa Stars baada ya wa kwanza kuifunga Niger 1-0 ugenini huku Morocco yenyewe ikicheza mchezo wa kwanza baada ya ule wa awali dhidi ya Eritrea kutofanyika kutokana na wapinzani wao kujitoa.

Katika kundi hilo, Zambia inaongoza ikiwa na alama 3 na mabao mawili iliyowafungwa Congo Brazaville na Stars ikifuatia ikiwa na alama kama hizo ila zinatofautiana kwa mabao.

Mshindi wa kila kundi ndio atafuzu moja kwa moja kwenye michuano ya Kombe la Dunia 2026 ambayo inatarajia kufanyika Mexico na Canada.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Pulsesports, Kocha wa Stars, Amrouche, amesema wapo kwaaajili ya kuwafurahisha mashabiki wao kwa kupata ushindi, hivyo watajitahidi kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.

“Tuna wachezaji wazuri na tunaendelea kuwapa mbinu za kuhakikisha tunatengeneza nafasi nyingi na kupata mabao mengi ili kuwapa furaha mashabiki wetu,” amesema.

Kwa upande wa Golikipa wa Stars, Aishi Manula ambaye anaichezea Simba, amesema wanafahamu wanaenda kukutana na timu bora kwenye Bara la Afrika ila watapambana kupata matokeo mazuri.

Aidha amewaomba watanzania kujitokeza kwa wingi kuwaunga mkono lakini kuunga mkono juhudi za Rais Samia za kuhakikisha kwamba Tanzania inafanya vizuri.

Kwa upande wa Kocha wa Morocco, Regragui, ameshukuru kwa mapokezi ya watanzania na kwamba ili mtu afuzu ni lazima ashinde, hivyo watahakikisha wanashinda.

“Tunaiheshimu Tanzania kwasababu tunajua wapo nyumbani wana morali ya kutosha na hata matokeo yao ya mchezo uliopita yanawawapa imani kubwa ya kufanya vizuri,” amesema.

Tags: