Kocha wa Azam FC Yusuph Dabo akiri ushindi wa 5-0 ulikuwa mgumu

Wachezaji wa Azam, Ayoub Lyanga (kushoto) na Kipre Junior, wakishangilia moja ya mabao yao

KANDANDA Kocha wa Azam FC Yusuph Dabo akiri ushindi wa 5-0 ulikuwa mgumu

Na Zahoro Juma • 18:23 - 23.02.2024

Ni baada ya kuifunga Green Warrior's na kutinga 16 Bora ya michuano ya ASFC

Licha ya kuitandika Green Warrior's mabao 5-0 katika michuano ya Azam Federation Cup (ASFC), Kocha wa Azam FC, Yusuph Dabo, amesema mechi haikuwa rahisi kutokana na aina ya wapinzani wao.

Mchezo huo uliokuwa wa raundi ya tatu ya michuano hiyo, umeifanya Azam kutinga 16 Bora ambayo sasa itaumana na Mtibwa Sugar.

Mabao ya Idd Suleiman Nado dakika ya 32, Kipre Junior dakika ya 33, Paul Kyabo dakika ya 56 alijifunga, Abdul Sopu dakika ya 65 na Ayoub Lyanga dakika ya 83, yalitosha kuipa ushindi mnono timu hiyo.

Mtibwa Sugar ilipenya hatua hiyo kwa ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Stand United katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Manungu, Morogoro.

Akizungumza na Pulsesports baada ya kumalizika kwa mchezo huo usiku wa jana, Dabo amesema alijua mchezo utakuwa mgumu kutokana na hatua iliyofikia.

"Haikuwa rahisi kupata ushindi huo mnono, hizi mechi inatakiwa kuchanga vizuri karata zako na timu zingine huwa zinakuja kwa kutaka kupoteza muda ili ufike wakati wa kupigiana penalti," amesema Dabo.

Amesema walijipanga na kuhakikisha wanapata mabao ya mapema kitu ambacho walifanikiwa na hatimaye kusonga mbele hatua inayofuata.

Ameongeza ni michuano inayohitaji umakini mkubwa ili kusonga mbele na ndio maana walijipanga kupanga kikosi kizuri kitakacholeta matokeo mazuri kwani bado wana mechi nyingi za kucheza katika mashindano mbalimbali.

Mchezo mwingine uliopigwa jana katika michuano hiyo, JKT Tanzania iliitandika TMA Stars 5-1.

Tags: