Kocha Simba adai uwanja sababu kushinda 1-0

KANDANDA Kocha Simba adai uwanja sababu kushinda 1-0

Na Zahoro Juma • 21:33 - 16.02.2024

Kauli hiyo imetolewa na Kocha Msaidizi, Daniel Cadena baada ya timu yake kuifunga JKT Tanzania

Kocha Msaidizi wa timu ya Simba SC, Daniel Cadena, amesema walilazimika kubadilisha mbinu wakati wanacheza na JKT Tanzania kutokana na mazingira ya uwanja.

Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa ligi waliocheza na JKT Alhamisi katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Hata hivyo katika mchezo huo, Simba ilionekana kuzidiwa katika sehemu kubwa ya mchezo huku nafasi kubwa waliopata ni hiyo ambayo Clatous Chama alifunga bao kipindi cha kwanza.

"Hatukuwa katika hali ya utulivu, tulijaribu kucheza aina yetu ya mpira lakini ilishindikana hivyo tulilazimika kucheza kwa aina tofauti," amesema.

Ushindi huo kwa Simba ni wa nne katika mechi tano zilizopita tangu ligi iliporejea baada ya mapumziko ya kupisha michuano ya Afcon.

Hivi sasa Simba imebakisha alama nne tofauti na vinara wa ligi hiyo, Yanga na ikiwa timu zote zimecheza mechi 15.

Simba inatarajia kurudi uwanjani Jumapili ambapo itacheza na Mtibwa Sugar katika mechi yao ya kwanza duru la pili.

Tags: