Kocha Ouma aanza na ushindi Coastal Union

KANDANDA Kocha Ouma aanza na ushindi Coastal Union

Na Zahoro Mlanzi • 20:22 - 23.11.2023

Huo ndio mchezo wake wa kwanza wa kimashindano tangu arithi mikoba ya Mwinyi Zahera

Klabu ya Coastal Union ya mkoani Tanga, imeibuka na ushindi ugenini wa bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Bara.

Hiyo ni mechi ya kwanza kwa Kocha Mkenya, David Ouma tangu arithi mikoba iliyoachwa na Mwingi Zahera ndani ya timu hiyo.

Ushindi huo, umeifanya Coastal kufikisha alama 10 na kupanda hadi nafasi ya 10 katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa imecheza mechi 10 huku Prisons ikibaki nafasi ya 15 na alama zao 7.

Bao pekee kwenye mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya, limefungwa kipindi cha kwanza na Roland Beakou dakika ya 17 akiunganisha mpira wa kona uliopigwa na Lucas Kikoti.

Kocha Ouma ana uzoefu wa zaidi ya miaka 15, amepita katika Kituo cha Michezo cha Ajax cha nchini Uholanzi, ana Leseni ya UEFA na Leseni A ya CAF na pia amewahi kupata mafanikio ndani ya Klabu ya Sofapaka na timu ya Taifa ya Kenya 'Harambee Stars'.

Ouma ni kocha anayeheshimika ndani ya Kenya na amefanya kazi kwa muda mrefu na kikosi cha Sofapaka akiwa ameitumikia katika nafasi tofauti ikiwemo nafasi ya Mkurugenzi wa Ufundi.

Kocha huyo sasa atalazimika kuelekea nguvu katika mchezo ujao dhidi ya Singida Fountain Gate utakaopigwa Novemba 27 kwenye Uwanja Liti mkoani Singida.

Tags: