Kocha Geita Gold aachia ngazi bila kutimuliwa

LIGI KUU Kocha Geita Gold aachia ngazi bila kutimuliwa

Na Zahoro Mlanzi • 21:45 - 20.12.2023

Huyo anakuwa ni kocha wa 12 kuachia ngazi tangu kuanza kwa ligi hiyo msimu wa 2023/24

Kocha Hemed Suleiman 'Morocco', ameomba kuacha kazi ya kukinoa kikosi cha Geita Gold FC kwa madai kuwa amebanwa na majukumu ya timu ya Taifa 'Taifa Stars'

Kocha huyo alijiunga na Geita Gold tangu mwanzo wa msimu huu huku akiwa pia ni kocha msaidizi wa Stars akimsaidia majukumu Kocha, Adel Amrouche.

Hivi karibuni kikosi cha Taifa Stars kinatarajia kuingia kambini kwa ajili ya kujiwinda na michuano ya Afcon ambayo inatarajia kuanza kutimua vumbi mapema mwezi ujao nchini Ivory Coast.

Hata hivyo tangu Morocco achukuwe mikoba ya Geita akirithi nafasi ya Fred Minziro mambo yamekuwa hayaendi vizuri wakati huu ambapo timu imecheza michezo 12 na wamekusanya alama 13 huku wakiwa wanashika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi.

Kocha anayetajwa kuja kuziba nafasi ya Morocco ndani ya Geita ni Denis Kitambi ambaye naye hivi karibuni aliacha kazi ya kukinoa kikosi cha Namungo ya mkoani Lindi.

Kupitia ukurasa wao rasmi wa klabu hiyo, wamethibitisha taarifa hiyo na kumtakia kila la kheri Kocha Morocco ambaye pia anahusishwa na nafasi iliyowazi ndani ya kikosi cha Ihefu FC ya mkoani Mbeya.

"Kwa makubaliano ya pande mbili tumeamua kuachana na Kocha, Hemed Suleiman ili kumpa wakati mzuri wa majuku ya timu ya taifa," imesomeka taarifa ya klabu hiyo," alisema. 

Morocco atakuwa ni kocha wa 12 kuachia ngazi katika ligi hiyo ikiwa inakwenda katika mzunguko wa 14 huku timu zingine zikiwa katika mzunguko wa 9 kutokana na majukumu ya mechi za kimataifa.

Ukiachana na Geita, timu zingine ambazo ziliachana na makocha wao ni Singida Fountain Gate, Simba SC, Namungo, Ihefu, Mtibwa Sugar na Prisons ya Mbeya.

Tags: