Kocha Chabruma, Najiati watajwa Tuzo za CAF

KANDANDA Kocha Chabruma, Najiati watajwa Tuzo za CAF

Na Zahoro Mlanzi • 13:00 - 15.11.2023

Wawili hao wameisaidia timu ya JKT Queens kufuzu michuano ya Klabu Bingwa Afrika upande wa wanawake licha ya kuishia hatua ya makundi

Licha ya timu yake kuishia katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake 2023, Kocha wa timu ya JKT Queens, Esther Chabruma na mlinda lango wake, Najiati Idrisa, wameteuliwa kuwania tuzo za Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Wawili hao wamepata mafanikio makubwa wakiwa na timu hiyo msimu uliopita baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake ya Tanzania ikiwa ni mara kwanza kwa klabu hiyo.

Mbali na mafanikio hato lakini wawili hao pia wameisaidia timu yao kufuzu michuano ya Klabu Bingwa Afrika upande wa wanawake ambayo inaendelea nchini Ivory Coast lakini wakiwa wameishia hatua ya makundi.

Kwenye michuano hiyo, JKT Queens walipangwa kundi moja na wenyeji Athletico Abidjan, Mamelod Sundowns Ladies na Sporting Casablanca na walijikuta wakimaliza nafasi ya tatu.

Pia JKT Queens, imeingia 10 Bora ya timu ambazo zinawania tuzo ya Timu Bora ya klabu kwa upande wa wanawake na hii ni kutokana na mafanikio waliyopata msimu uliopita na huu unaoendelea.

Kwa upande wa timu ya Taifa ya Wanawake ya 'Twiga Stars', nao wameingia katika kuwania tuzo ya Timu Bora ya Taifa ya mwaka.

Tuzo hizo zinatarajiwa kutolewa nchini Morocco ifikapo Desemba 11, mwaka huu.

Tags: