Kocha Azam akoshwa sapoti ya mashabiki ugenini

KANDANDA Kocha Azam akoshwa sapoti ya mashabiki ugenini

Zahoro Mlanzi • 22:00 - 02.11.2023

Katika mchezo huo hadi mapumziko timu hizo zilikuwa hazijafungana na kusababisha hofu pengine Azam itapoteza mchezo wa tatu mfululizo.

Kocha Msaidizi wa Azam FC, Bruno Ferry, amesema ushindi waliopata dhidi ya Mashujaa FC kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika umetokana na mashabiki wao waliojitokeza kwa wingi kuwaunga mkono.

Akizungumza na Pulse Sportsbaada ya mchezo huo ambao Azam ilishinda 3-0, Ferry amesema haukuwa mchezo rahisi lakini mashabiki walikuwa nyuma yao hadi mwisho.

Katika mchezo huo hadi mapumziko timu hizo zilikuwa hazijafungana na kusababisha hofu pengine wakapoteza mchezo wa tatu mfululizo.

Hata hivyo, mapema kipindi cha pili winga Kipre Jr alifungua ukurasa wa mabao kwa kufunga bao la uongozi wa Azam akiunganisha pasi safi ya Gibrill Sillah.

Sillah alifunga bao la pili akiitumia pasi ya Feisal Salum ambaye naye alitengeneza bao la tatu kwa Alassane Diao .

Ushindi huo umewarudisha Azam kwenye nafasi ya tatu baada ya kufikisha alama 16 wakiwa wameshuka dimbani mara nane msimu huu.

"Mchezo ulikuwa mgumu na tulihitaji mashabiki wa aina hii ili kuweza kushinda mchezo," amesema Kocha Ferry.

"Haikuwa vizuri hasa ukiangalia tumetoka kupoteza mechi mbili mfululizo, hivyo tulihitaji matokeo ya ushindi ili kujiweka sawa," amesema.

Azam sasa wanatarajia kushuka dimbani Jumamosi kwenye Uwanja wa Highland Estate mkoani Mbeya kwa ajili ya kucheza dhidi ya Ihefu ambao nao wametoka kupata sare ugenini dhidi ya Singida FG. 

Fuatilia Pulse Sports Kenya kwenye WhatsApp kwa habari zaidi.

Tags: