Klabu ya Azam FC yapata pigo kubwa baada ya kipa Ahamada kuumia

KANDANDA Klabu ya Azam FC yapata pigo kubwa baada ya kipa Ahamada kuumia

Na Zahoro Mlanzi • 21:00 - 15.12.2023

Kipa huyo wa Azam FC anayetokea visiwa vya Comoro, anakuwa ni kipa wa pili kuumia ndani wa timu hiyo msimu huu

Klabu ya Azam FC, imepata pigo baada ya kipa wake Mcomoro, Ali Ahamada kuumia na kufanya sasa ibakiwe na kipa wa tatu pekee Zuberi Foba Masoud ambaye ni zao la timu za vijana.

Tayari Ahamada, 32, amesafirishwa usiku wa kuamkia leo kwenda jijini Cape Town, Afrika Kusini kufanyiwa uchunguzi wa goti lake la mguu wa kushoto aliloumia katika Hospitali ya Vincent Pallotti.

Kipa huyo raia wa Ufaransa, alipata maumivu hayo katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya KMC ambao Azam FC ilishinda 5-0 Desemba 7 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Hata hivyo, baada ya matibabu ya awali, Ahamada amepata nafuu na kumudu kucheza mchezo uliofuata dhidi ya JKT Tanzania Desemba 11, ambao Azam FC ilishinda 2-1, kabla ya maumivu hayo kuzidi hadi kusafirishwa Afrika Kusini kwa matibabu.

Huyo anakuwa kipa wa pili wa Azam FC kuumia hadi kupelekwa Afrika Kusini kwa matibabu baada ya Mghana Iddrisu Abdulai (26), aliyefarishwa kufanyiwa uchunguzi zaidi wa maumivu ya bega lake la mkqono wa kushoto.

Azam kwa sasa inaongoza Ligi hiyo ikiwa na alama 28 ikifuatiwa na Yanga yenye alama 24.

Pia Kiungo wao, Feisal Salum 'Fei Toto', anaongoza kwa upachikaji mabao akiwa ameweka kambani mabao 7 sawa na Jean Baleke wa Simba, Max Nzengeli na Stephen Azizi KI wote wa Yanga.

Tags: