Kitambi awa kocha wa 11 kutimuliwa

LIGI KUU Kitambi awa kocha wa 11 kutimuliwa

Na Zahoro Mlanzi • 16:13 - 13.12.2023

Kocha huyo alikuwa akiinoa Namungo FC ambayo katika msimu huu wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, imekuwa haina mwenendo mzuri

Uongozi wa Klabu ya Namungo ya mkoani Lindi, umetangaza kuachana na kocha wao, Denis Kitambi huku taarifa mbalimbali zikadai kuwa huenda akatambulishwa katika klabu ya Geita Gold ya mkoani Geita.

Kitambi ameondolewa Namungo ikiwa zimepita siku chache baada ya timu hiyo kutoka kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar katika michuano ya Ligi Kuu Bara.

Huyo anakuwa ni kocha wa 11 kutimuliwa msimu huu baada ya timu za Simba SC, Singida FG, Ihefu, Mtibwa Sugar, Tanzania Prisons, Coastal Union na Dodoma Jiji kufanya hivyo hapo awali.

Taarifa hiyo imekuja huku Namungo ikiwa katika maandalizi ya mchezo wao unaofuata wa ligi hiyo ambao watacheza Desemba 21 na Tanzania Prisons.

Namungo ipo katika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi wakiwa na alama 17 baada ya kushuka dimbani mara 13.

Msimu huu, Namungo ilianza ligi ikiwa chini ya Kocha, Mrundi Cedric Kaze ambaye alijiengua baada ya mechi tano za mwanzo kutokana na matokeo mabovu.

Ndani ya mechi hizo tano, Namungo walikuwa hawajashinda hata mechi moja. Timu hiyo ilipata ushindi wao wa kwanza msimu huu chini ya Kocha Kitambi kwa kuifunga Azam FC 3-1 ugenini.

Tangu hapo Namungo wamepata ushindi katika mechi nne nyingine ikiwemo mechi yao ya mwisho ya Desemba 7 ambapo waliifunga Mtibwa.

"Namungo FC inapenda kumshukuru Kocha Denis Kitambi kwa muda ambao ameitumikia timu yetu kwa ushirikiano mkubwa," imesomeka taarifa ya klabu hiyo kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii.