Kaze: Sihofii kutimuliwa Namungo FC

LIGI KUU: Kaze: Sihofii kutimuliwa Namungo FC

Na Zahoro Mlanzi • 19:08 - 22.10.2023

Namungo ilianza ligi hiyo kwa kufungwa bao 1-0 na JKT Tanzania, ikatoka sare 1-1 na KMC, ikafungwa 1-0 na Yanga, ikatoka suluhu na Mashujaa FC na ikatoka sare ya 1-1 na Kagera Sugar.

Kocha wa timu ya Namungo FC ya Ruangwa mkoani Lindi, Cedric Kaze, amesema hana hofu na kibarua chake licha ya kuwa hawajaanza vizuri msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara

Namungo ambayo Jumamosi wakiwa kwenye Uwanja wao wa Majaliwa, wamekubali kichapo cha 3-2 kutoka kwa Singida FG, kwasasa wanashika nafasi ya 14 wakiwa na alama 3 ndani ya mechi sita walizocheza na hawajashinda mechi yoyote msimu huu.

Mabao ya Singida Big Stars, yamefungwa na viungo Mkenya, Duke Abuya dakika ya 45 na Mtogo, Marouf Tchakei mawili dakika ya 68 na 81, wakati ya Namungo FC yamefungwa na Derick Mkombozi dakika ya 64 kwa penalti na Emmanuel Charles dakika ya 90.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Kaze ambaye msimu uliopita alikuwa kwenye kikosi cha Yanga akiwa ni msaidizi wa Kocha Nasredein Nabi, amesema bado anapata ushirikiano kutoka kwa viongozi wa juu na kwamba ana uhakika matokea yataanza kupatikana hivi karibuni.

"Hatujaanza vizuri msimu lakini tunafanya kila jitihada kuhakikisha kuwa mambo yanabadilika haraka iwezekanvyo," amesema.

"Jambo zuri ni kwamba bado napata ushirikiano mzuri kutoka kwa viongozi na hiyo inanipa nguvu ya kufanya kazi kwa bidii," amemalizia Kaze.

Baada ya kufungwa na Singida FG, Namungo sasa wanafunga safari kwenda Dar es Salaam ambapo Ijumaa watakuwa ni wageni wa Azam kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Namungo ilianza ligi hiyo kwa kufungwa bao 1-0 na JKT Tanzania, ikatoka sare 1-1 na KMC, ikafungwa 1-0 na Yanga, ikatoka suluhu na Mashujaa FC na ikatoka sare ya 1-1 na Kagera Sugar.

Tags: