Kocha huyo wa Yanga ametoa kauli hiyo baada ya kuiongoza timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya KMC
Kocha wa timu ya Yanga SC, Miguel Gamondi, amesema hesabu zake sasa zinahamia katika michezo ya kimataifa ambapo wiki ijayo anakabiliwa na mchezo muhimu wa kuamua hatima yao dhidi ya CR Belouizdad.
Gamondi amesema hayo mara baada ya kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya KMC katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliofanyika Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
"Kwa sasa akili zetu tunazihamishia kwenye ligi ya mabingwa, hatuna muda mrefu kabla ya kuanza kucheza michezo muhimu iliyosalia katika hatua ya makundi," amesema.
Yanga wanafukuzia kucheza hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza katika historia ya timu yao.
Hata hivyo, wanakabiliwa na mechi mbili muhimu za maamuzi ambapo watacheza mechi ya kwanza Februari 24 dhidi ya CR Belouizdad kabla ya kumaliza na Al Ahly, Machi Mosi.
Katika msimamo wa kundi lao hadi sasa wanashika nafasi ya tatu nyuma ya vinara Al Ahly wenye alama alama sita wakati Belouizdad wenyewe wana alama tano sawa na Yanga.
Katika Lgi Kuu, Yanga ni vinara wakiwa na alama 43 baada ya kushuka dimbani katika mechi 16 msimu huu.
Katika hatua nyingine, kocha huyo, amewamwagia sifa vijana wake kwa kuonesha ukomavu wao hasa katika nyakati ngumu walizopita hivi karibuni.
Amesema mechi kadhaa nyuma hazikuwa nzuri kwao kwa upande wa kiwango lakini kikubwa walikuwa wanapata alama tatu.
Hata hivyo amesema malengo hayo yalitimizwa na vijana wake ambao walionesha ukomavu wao kimpira kitu ambacho hakikuweza kuwa na usumbufu.
"Tulikuwa hatuchezi vizuri lakini ukomavu wa wachezaji wangu ulituwezesha kupata matokeo kitu ambacho ni muhimu zaidi," amesema.