Gamondi atangaza vita kwa Al Ahly

KANDANDA Gamondi atangaza vita kwa Al Ahly

Na Zahoro Juma • 16:00 - 25.02.2024

Kocha huyo wa Yanga SC, ametoa kauli hiyo baada ya kuiongoza timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya CR Belouizdad akitaka kuongoza kundi

Kocha wa timu ya Yanga SC, Miguel Gamondi, amewatangazia kiama Al Ahly katika vita ya kusaka nafasi ya kuongoza msimamo wa Kundi D.

Wawili hao wanatarajia kufunga hesabu za mechi za makundi kwa mchezo wa mwisho utakaochezwa Machi Machi Mosi nchini Misri.

Yanga ipo nafasi ya pili wakiwa na alama 8 huku Al Ahly wao ni vinara wa Kundi D baada ya kukusanya alama 9 katika michezo mitano.

Mshindi katika mechi ya mwisho atajihakikishia nafasi ya kuongoza kundi na kupata ‘pot 1’ katika droo ya upangaji wa hatua ya robo fainali ambapo faida yake itakuwa ni kuanzia ugenini.

Akizungumza mara baada ya mchezo wa CR Belouizdad ambao waliibuka na ushindi wa mabao 4-0, Gamondi amesema kama kawaida yake yeye kila mchezo huwa anajiandaa kutafuta ushindi.

Amesema ushindi ni kitu muhimu kwake kwenye mchezo huo licha ya kukiri kuwa wapinzani wake ni wagumu hasa wanapokuwa nyumbani.

"Kama unanijua vizuri mimi kila mechi huwa najiandaa kwa ajili ya ushindi, tutapanga mipango yetu vizuri lakini pia tunatambua kazi kubwa iliyopo kwenye mchezo huo," amesema.

Aidha alijivunia uzoefu wake kwa soka la uarabuni na kusema huwa inamsaidia kuwatambua wapinzani hasa wanaotoka Afrika Kaskazini.

Akizungumzia kuhusu mchezo dhidi ya Belouizdad, amesema alijiandaa kushinda lakini hakudhani kama wangeweza kufunga mabao manne kwenye mchezo huo kutokana na ubora wa wapinzani wao.

"Nilijua kama tutashinda lakini sikutajia kama zitafika bao nne kwa kweli, najivunia vijana wangu wameonesha moyo wa kujituma," amesema Gamondi ambaye aliwahi kufundisha CR Belouizdad.

Yanga imefuzu hatua ya robo fainali ikiwa ni kwa mara ya kwanza katika historia ya timu yao tangu ilipoanzishwa miaka 89 iliyopita.

Mafanikio haya yanakuja ikiwa ni msimu uliopita tu wakiwa wametoka kucheza hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo walipoteza mbele ya USM Alger.

Tags: