FIFA yaifungia Singida FG ya Tanzania kusajili

© Singida FG

KANDANDA FIFA yaifungia Singida FG ya Tanzania kusajili

Zahoro Mlanzi • 21:03 - 14.11.2023

Adhabu hiyo imetokana na Nicholas Gyan amefungua kesi akiidai klabu hiyo fedha ya ada ya uhamisho pamoja na malimbikizo ya mshahara wa miezi kadhaa

Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (Fifa), limeifungia Klabu ya Singida FG ya Tanzania kusajili hadi watakapomlipa aliyekuwa mchezaji wao, Mghana Nicholas Gyan.

Adhabu hiyo imetolewa baada ya Gyan kushinda kesi ya madai dhidi ya klabu hiyo yenye maskani yake mkoani Singida.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Gyan ambaye amewahi kuitumikia pia klabu ya Simba, amefungua kesi akiidai klabu hiyo fedha ya ada ya uhamisho pamoja na malimbikizo ya mshahara wa miezi kadhaa.

Awali FIFA wamewaamuru Singida FG wamlipe mchezaji huyo stahiki zake ndani ya siku 45 kitu ambacho hakikutekelezwa na kusababisha uamuzi huo.

Kutokana na adhabu hiyo ya FIFA, pia TFF, imeifungia Singida kufanya usajili wa ndani.

Kama Singida hawatoweza kulipa deni hilo basi hawataweza kusajili mchezaji yoyote katika dirisha la usajili linalotarajiwa kufunguliwa Desemba 15.

Tags: