David Ouma apania kumaliza Nne Bora na Coastal Union

LIGI KUU David Ouma apania kumaliza Nne Bora na Coastal Union

Na Zahoro Juma • 11:00 - 22.02.2024

Ni baada ya kupata matokeo mazuri katika mechi zake tano mfululizo tangu aliporithi mikoba ya Mkongo, Mwinyi Zahera ya kuinoa Coastal Union

Kocha wa kikosi cha Coastal Union, Mkenya David Ouma, amesema timu yake ina uwezo wa kuchukuwa nafasi nne za juu ambazo zitawawezesha wao kucheza mechi za kimataifa msimu ujao.

Coastal Union wapo nafasi ya nne hadi sasa kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara wakiwa na alama 23 ambapo mechi za mzunguko wa pili zimeshaanza.

Ouma amesema hayo na Pulsesports wakati huu akijiandaa na mechi inayofuata ya ligi ambapo Coastal Union wanatarajia kuwakaribisha Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani Jumamosi.

"Wachezaji wangu wanafanya vizuri na hiyo inanitimia moyo kwamba tunaweza kusalia ndani ya timu nne za juu hadi kufikia mwisho wa msimu huu," amesema.

Kocha huyo alikuja katikati ya msimu ambapo alichukuwa nafasi ya Kocha Mwinyi Zahera ambaye alianza msimu kabla ya mambo kumuendelea kombo.

Tangu kaingia kazini kocha huyo timu imeonekana kuwa katika mabadiliko makubwa ambapo hadi sasa timu hiyo ipo katika mfululizo wa kucheza mechi tano bila kufungwa.

Mbali na hiyo lakini wamekuwa na safu nzuri ya ulinzi ambayo imemuwezesha Kipa wao, Ley Matampi kuwa kinara wa 'clean sheet' katika ligi hiyo.

Katika msimamo wa ligi hiyo, Coastal inashika nafasi ya nne ikiwa na alama 23 baada ya kucheza mechi 16 huku ikitanguliwa na Simba SC, Azam FC na vinara Yanga SC.

Tags: