Bangala azua hofu Azam FC

© Kwa hisani

KANDANDA Bangala azua hofu Azam FC

Zahoro Mlanzi • 20:16 - 05.10.2023

Kiungo wa Azam FC, Yannick Bangala, ameumia nyama za paja katika mechi na hajulikani muda wa kupona

Kiungo Mkongo wa timu ya Azam FC, Yannick Bangala, ameshanika nyama za paja na bado haijajulikana atakuwa nje ya uwanja kwa muda gani.

Bangala ambaye alisajiliwa na timu hiyo akitokea kwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Yanga, amepata tatizo hilo wakati wa mechi yao dhidi ya Dodoma Jiji iliyomalizika kwa suluhu.

Kiungo huyo anaungana na wachezaji wengine kama straika Prince Dube na kiungo, Yahya Zayd katika benchi la majeruhi.

Taarifa ya Azam FC imeeleza kwamba baada ya mechi hiyo, Bangala alirejea Dar es Salaam kwa vipimo zaidi, wakati timu ikienda jiji Tanga kwa ajili ya mchezo wa Ijumaa dhidi ya Coastal Union.

“Baada ya vipimo ndiyo itajulikana ukubwa wa tatizo na muda wa matibabu hadi kupona,” imesema taarifa ya Azam FC.

Katika mchezo huo uliopigwa Dodoma, Bangala alikuwa mhimili mkubwa kwa Azam katika eneo la kiungo akishirikiana na Feisal Salum na Sospeter Bajana na kuwapa wakati mgumu wapinzani wao.

Kutoka kwake ambapo nafasi ilichukuliwa na Ayoub Lyanga kuliifanya timu yake kuwa na wakati mgumu kwa Dodoma Jiji kuanza kuliandama lango lao.

Hata hivyo, Kocha wa timu hiyo, Youssouph Dabo, akizungumzia kuumia kwa Bangala, amesema ni pigo kwa timu yake lakini wataendelea kuboresha safu ya kiungo kwani ana wachezaji wenye uwezo mkubwa.