Azam FC yatinga robo fainali Mapinduzi Cup

KANDANDA Azam FC yatinga robo fainali Mapinduzi Cup

Na Zahoro Mlanzi • 20:40 - 02.01.2024

Imetinga hatua hiyo baada ya kujikisanyia alama 7 katika michuano hiyo ndani ya michezo mitatu

Timu ya Azam FC, imekata tiketi ya robo fainali ya michuano ya Mapinduzi Cup baada ya kuifunga Vital'O ya Burundi kwa mabao 3-1.

Mchezo huo umechezwa Uwanja wa New Amani Complex, visiwani Zanzibar. 

Mshambuliaji wa Azam, Allasane Diao, amefunga mabao mawili huku bao moja likifungwa na Pascal Msindo. Bao la Vital'O lilifungwa kwa mkwaju wa penati na nahodha wao Jean Nzeyimana.

Katika mchezo huo, Diao ametangazwa kuwa nyota wa mchezo kutokana na mchango wake wa kufunga mabao mawili.

Mabao hayo mawili yamewafanya Diao kuwa kinara wa mabao akifikisha mabao matatu sambamba na Mkenya, Elvis Rupia wa Singida FG.

Azam wamekamilisha mechi zao tatu za makundi wakiwa wamekusanya alama 7 huku wakifuatiwa na Vital'O wenye alama mbili na wote wamemaliza mechi zao.

Klabu ya Chipukizi na Mlandege wao watacheza mechi ya mwisho ambayo itaamua nani aungane na Azam kwenye hatua inayofuata.

Tags: