Azam FC yapata pigo, nyota wawili 'out'

© Kwa Hisani

KANDANDA Azam FC yapata pigo, nyota wawili 'out'

Zahoro Mlanzi • 13:11 - 02.10.2023

Wachezaji hao wanaendelea na programu ya kutibu majeraha yao chini ya uangalizi wa Mtaalamu wa tiba za viungo wa timu, Joao Rodrigues.

Timu ya Azam FC, imepata pigo baada ya wachezaji wake nyota wawili, straika Prince Dube na kiungo, Yahya Zayd kuumia na kuwa nje ya uwanja kwa wiki tatu.

Wachezaji hao walilazimika kufanyiwa mabadiliko ya haraka kipindi cha kwanza wakati Azam FC ilipoichapa Singida Fountain Gate mabao 2-1, kwenye mchezo uliopita wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Dube anasumbuliwa na majeraha ya nyonga, huku Zayd akiwa amepata majeraha katika goti lake.

Wachezaji hao wanaendelea na programu ya kutibu majeraha yao chini ya uangalizi wa Mtaalamu wa tiba za viungo wa timu, Joao Rodrigues.

Akizungumzia maendeleo ya wachezaji hao, Kocha wa timu hiyo, Youssouph Dabo, amesema ni pengo kubwa kwake kuelekea mchezo wao ujao dhidi ya Dodoma Jiji ugenini.

"Ni pengo kwani ni wachezaji wetu muhimu, tuna mechi ngumu Oktoba 3 jijini Dodoma, hivyo kuwakosa kipindi hiki inaumiza lakini hakuna jinsi tuna kikosi kipana tutaendelea kuwaandaa ili tufanye vizuri kwenye mchezo huo," amesema Dabo.

Azam itashuka uwanjani siku hiyo kuumana na Dodoma Jiji katika mchezo utakaopigwa kuanzia saa 1 usiku Uwanja wa Jamhuri jijini humo.

Katika msimamo wa ligi hiyo, Azam inashika nafasi ya tatu ikiwa na alama 9 sawa na vinara wa ligi hiyo, Yanga SC na Simba SC.