Ni baada ya kusawazisha bao kipindi cha pili na kufungana 1-1
Matumaini ya Azam FC kuwania ubingwa msimu huu yanaendelea kuingia doa baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Tanzania Prisons katika mchezo wa ligi uliofanyika katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Hiyo inakuwa ni sare ya pili mfululizo kwa Azam mara baada ya kulazimishwa suluhu katika mchezo wao uliopita wa ligi dhidi ya Tabora United.
Dhidi ya Prison, timu ya Azam walijikuta katikati ya mshtuko baada ya kutanguliwa kwa bao la mapema kipindi cha kwanza kupitia kwa Samson Mbangula ambaye alipiga mkwaju mkali nje ya boksi dakika ya nne ya mchezo.
Bao hilo lilidumu hadi mapumziko huku kila timu ikionekana kucheza kwa nidhamu kitu kilichosababisha uchache wa nafasi kwenye kipindi cha kwanza.
Azam ilifanikiwa kurejesha bao hilo kipindi cha pili kupitia kwa kiungo wao, Feisal Salum aliyefunga kwa mkwaju wa penalti baada ya beki Jumanne El-Fadhil kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari.
Matokeo hayo, yanawaacha Azam wakiwa katika nafasi ya pili na michezo 17 na alama 37 ambazo ni sita nyuma ya Yanga ambao ni vinara wakiwa wamecheza mechi 16.
Matokeo mengine;
Tabora United 1-1 Singida FG
Geita Gold 1-3 Mashujaa