Azam FC yakana kumtimua Kocha Dabo

SOKA Azam FC yakana kumtimua Kocha Dabo

Zahoro Mlanzi • 15:15 - 01.11.2023

Taarifa nchini zinadai wachezaji wa Azam hawavutiwi na ufundishaji wa kocha huyo na kwamba wanashinikiza afutwe kazi.

Uongozi wa kikosi cha timu ya Azam FC, umemkingia kifua Kocha wao raia wa Senegal, Yusuph Dabo, kwa kusema bado yupo sana ndani ya timu hiyo.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari nchini vinadai wachezaji wa Azam hawavutiwi na ufundishaji wa kocha huyo na kwamba wanashinikiza afutwe kazi.

Hata hivyo Pulsesports, imezungumza na Ofisa Habari wa klabu hiyo, Hashim Ibwe kujua ukweli wa suala hilo, ambaye amesema kocha huyo bado yupo klabuni na taarifa zote kuhusu yeye ni uzushi.

Amesema kwasasa kocha huyo anakiandaa kikosi chake ili kuweza kutimiza malengo mbalimbali waliojiwekea msimu huu ikiwemo kushinda mataji katika michuano ambayo bado wanashiriki.

"Kocha wetu bado yupo na hata kambini kwetu hakuna kitu kama hicho, wachezaji wote wana maelewano mazuri na kocha ndio maana bado wanafuata kile anachowafundisha," amesema.

Taarifa za Dabo kukalia kuti kavu zimekuja mara tu baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Yanga SC na Namungo FC.

Kikosi cha Azam ambacho pia kiliondoshwa mapema kweye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika hadi sasa wapo kwenye nafasi ya nne kwenye msimamo wakiwa na alama 13 baada ya kushuka dimbani mara 7.

Kwasasa wanakabiliwa na mechi mbili za ugenini dhidi ya Mashujaa mchezo ambao unachezwa Novemba Mosi mkoani Kigoma na mechi itakayofuata ni dhidi ya Ihefu FC itakayopigwa Jumamosi.

Tufuate kwenye mtandao wetu wa kijamii wa WhatsApp ili uweze kupata ripoti zaidi kuhusu nyanja mbalimbali spoti.

Tags: