Azam FC sasa kujipima na JKU ya Zanzibar

KANDANDA Azam FC sasa kujipima na JKU ya Zanzibar

Na Zahoro Mlanzi • 19:03 - 17.11.2023

Awali timu hiyo ilitakiwa kuumana na Gor Mahia Jumapili na leo ndio ilikuwa ianze safari kwenda Kenya

Baada ya mchezo wa kirafiki wa kimataifa kati ya Azam FC na Gor Mahia ya Kenya kufutwa, matajiri hao wa Jiji la Dar es Salaam sasa watajipima kwa JKU ya visiwani Zanzibar.

Awali Azam ilitakiwa kuumana na Gor Mahia Jumapili na leo ndio ilikuwa ianze safari kwenda Kenya lakini imeshindikana kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wao.

Mechi hiyo ilipangwa kuchezwa Uwanja wa Kasarani uliopo jijini Nairobi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Azam FC, kutokana mchezo huo kufutwa sasa watacheza na JKU ya Zanzibar Jumapili Uwanja wa Azam Complex kuanzia saa 1:00 usiku.

"Hatutakuwa na mechi yetu ya kimataifa dhidi ya Gor Mahia ya Kenya kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo, hivyo badala yake tutacheza na JKU ya Zanzibar, tunawaomba mashabiki wetu kujitokeza kwa wingi siku hiyo uwanjani kwetu," imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Hata hivyo Pulse Sports, inaelewa mchezo huo umeshindwa kufanyika kutokana na Gor Mahia kupewa adhabu na kupigwa faini na Shirikisho la Mpira wa Miguu Kenya (FKF) kutokana na mashabiki wake kufanya vurugu na uharibifu uwanjani Kasarani wakati wa mechi yao dhidi ya Murang'a Seal.

Kutokana na uharibifu huo, Gor Mahia imepigwa faini ya shilingi milioni 2 za Kenya na itacheza mechi zao tano mfululizo bila mashabiki.