Timu hiyo kwa kwasasa ipo kambini jijini Dar es Salaam kujiandaa na mechi za mashindano mbalimbali yaliyopo mbele yao
Klabu ya Azam FC, inatarajia kucheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa Jumapili dhidi ya Klabu ya Gor Mahia ya Kenya.
Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa kuanzia saa 10 jioni kwa saa za Afrika Mashariki kwenye Uwanja wa Kasarani nchini Kenya ambapo kikosi cha Azam kinatarajia kuondoka nchini kesho.
Azam ambao kwasasa wapo kambini jijini Dar es Salaam, wanajiandaa kwa ajili ya mechi zijazo za Ligi Kuu Bara zinazotarajiwa kuendelea kuanzia Novemba 25 baada ya mapumziko kupisha timu za Taifa, watavaana na Mtibwa Sugar.
Akizungumza na Pulsesports, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Thabit Zakaria 'Zaka Zakazi', amesema wachezaji ambao hawakwenda kwenye timu zao za taifa wanaendelea vizuri na maandalizi kabla ya kuungana na wenzao hapo baadaye.
"Wachezaji wote waliobaki klabuni wanaendelea vizuri na maandalizi na kocha alipendekeza mchezo wa kirafiki ili kuwaweka wawe fiti kama wenzao ambao wamekwenda kwenye timu za taifa," amesema.
Amesema mchezo huo na Gor Mahia utasaidia katika kuendelea kukiangalia kikosi chao kabla ya kuanza mechi za ligi kuu.
Katika hatua nyingine, klabu hiyo, imefikia makubaliano ya kumuuza mchezaji wao kinda raia wa Tanzania, Cyprian Kachwele ambaye amejiunga na Klabu ya Vancouver Whitecaps FC.
Kachwele ni zao la timu za vijana wa Azam ambapo amecheza mechi mbambali kwa upande wa vijana kabla ya mwishoni mwa msimu uliopita kupandishwa timu ya wakubwa ambapo alicheza michezo mitatu.
Timu ya Vancouver pia amewahi kupita kiungo wa zamani wa Tanzania, Nizar Khalfan.