Nyota hao watakosekana kutokana na sababu mbalimbali wakati timu hiyo ikiondoka kesho jijini Dar es Salaam
Timu ya Simba SC, inatarajia kuondoka alfajiri ya kesho kwenda nchini Ivory Coast kuwafuata Asec Mimosa kwa ajili ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika unaotarajiwa kuchezwa Ijumaa.
Katika safari hiyo Simba, imelazimika kuwaacha nchini Mlinda lango Ayoub Lakred ambaye hataweza kucheza mchezo huo kutokana na kuwa na kadi tatu za njano pamoja na Willy Onana ambaye anasumbuliwa na nyama za paja.
Onana na Ayoub wote kwa pamoja walikuwa ni nyota mara ya mwisho wakati Simba wanacheza michuano hiyo dhidi ya Wydad Casablanca kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Desemba 19, mwaka jana.
Mchezo huo Simba, iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 ambayo yote yalifungwa na Onana lakini Ayoub alikuwa imara kwa kuokoa michomo ya hatari ambayo iliiweka timu yake salama hasa kipindi cha kwanza.
Akizungumzia maandalizi ya safari hiyo, Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema ukiachana na wachezaji hao lakini wengine wote wapo tayari kwa ajili ya safari na mchezo huo muhimu.
"Kikosi chote kipo tayari kwa ajili ya safari na mchezo, tunakabiliwa na mchezo mgumu lakini kwa muda ambao tumepewa wa kujiandaa tunaimani tutafanya vizuri," amesema.
Simba leo ilifanya mazoezi yao ya mwisho wakiwa jijini Dar es Salaam chini ya kocha Abdelhak Benchikha.
Simba, wenya alama tano katika Kundi B, watacheza na Asec ambao ni vinara wenye alama 10 na kimahesabu wanaonekana kuwa wameshakata tiketi ya kuvuka kwenda hatua ya robo fainali.
Simba ikifanikiwa kutinga hatua ya robo fainali itakuwa ni mara yao ya tano kwa miaka ya hivi karibuni katika ushiriki wao wa michuano ya kimataifa.