Tuzo hizo kwa upande wa ngumi ni za kwanza katika historia ya taifa la Tanzania na zinatarajiwa kuwa chachu kubwa katika kuwaamsha mabondia waweze kufanya vizuri.
Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) kwa kushirikiana na Kampuni ya Tosh Cargo, wameandaa tuzo kwa ajili ya mchezo wa ngumi ambazo zitafanyika Juni, mwakani huku Rais Dkt Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Baadhi ya mabondia katika uzito tofauti ambao wamekuwa wakifanya vizuri nchini ni Seleman Kidunda, Hassan Mwakinyo, Abdallah Pazi 'Dulla Mbabe', Ibrahim Class, Twaha Kiduku na Lulu Kayage, watakuwa sehemu ya watakaowania tuzo hizo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Tosh Cargo ambao ndio wadhamini wakuu, Amitin Mbamba, amesema lengo la tuzo hizo ni kwa ajili ya kutambua mchango na uwezo wa mabondia mbalimbali nchini.
Mbamba amesema kama Rais Samia atakubali kuitikia mwito wao basi wataandaa pambano fupi walau la raundi mbili ili kuweza kunogesha siku hiyo.
"Lengo letu ni kuongeza hamasa kwa wanamichezo hasa mabondia na ndio maana tumekuja na tuzo hizo ili kutambua uwezo wao," amesema Mbamba.
"Kwa mara ya kwanza tuzo hizi tutazifanya mwezi Juni mwakani na tunaomba Mheshimiwa Rais mama yetu Samia Suluhu Hassan awe mgeni rasmi."
Tuzo hizo kwa upande wa ngumi ni za kwanza katika historia ya taifa la Tanzania na zinatarajiwa kuwa chachu kubwa katika kuwaamsha mabondia waweze kufanya vizuri.