Amevunja rekodi hiyo baada ya kupanda hadhi ambapo kwasasa anashika nafasi ya saba duniani kati ya mabondia 1056 wa uzito wa Bantam
Bondia Fadhili Majiha, ameweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kuwa na nyota nne na nusu na kuvunja rekodi iliyowahi kuwekwa na mabondia Hassan Mwakinyo na Tony Rashid, kwa mujibu wa mtandao wa Boxrec.
Majiha amepandishwa hadhi hiyo baada ya hivi karibuni kutwaa ubingwa wa WBC Afrika uzito wa Bantam kwa kumchapa Bongani Mahlangu wa Afrika Kusini kwa pointi katika pambano la raundi 10 lililochezwa Ukumbi wa PTA, Dar es Salaam.
Majiha anakuwa mtanzania wa kwanza kufikia mafanikio hayo tangu nchi ya Tanzania kupata uhuru.
Mbali na kupata hadhi hiyo lakini pia kwasasa anashika nafasi ya saba duniani kati ya mabondia 1056 wa uzito huo 'kilo 54'.
Ikumbukwe mtanzania wa kwanza kufikia mafanikio kama hayo alikuwa ni Mwakinyo ambaye alifika hadhi ya nyota nne pamoja na kuingia katika 10 Bora akiwa nafasi ya tisa kwa uzito wa Super Walter 'kilo 67' na baadaye Rashid alifikisha nyota tatu na nusu na kuingia kwenye 20 Bora uzito wa Super Bantam 'kilo 57'.
Majiha amekuwa kwenye wakati mzuri tangu alipokuwa chini ya Kampuni ya HB Sadc Boxing Promotion ambao ndio waliomuandalia pambano lake hilo dhidi ya Bongani.